Utaratibu wa Rufaa
Uwasilishaji wa Rufaa Mbele ya Baraza
Mamlaka na Wigo wa Rufaa
Kwa mujibu wa Kifungu 136G (2) cha Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana [Sura ya 79], Baraza litakuwa na mamlaka ya kusimamia masuala yahusuyo;
- Kutafsiri utekelezaji au kanuni zozote zinazosimamiwa na sheria hii
- Migogoro baina ya Mamlaka na soko lolote la hisa
- Migogoro baina ya Mamlaka na dalali yoyote wa masoko
- Migogoro baina ya madalali wa masoko na wateja wao
- Migogoro baina ya makampuni yaliyoko kwenye masoko ya hisa na mamlaka za usimamizi au masoko ya dhamana
- Mamlaka kukataa maombi ya leseni
- Mamlaka kuweka ukomo au vizuizi kwenye leseni
- Mamlaka kufungia au kufuta leseni
- Kukataa kuidhinisha dhamana kwenye soko la hisa
- Kufungia uuzaji wa dhamana kwenye soko la hisa
- Kuiondoa dhamana kwenye orodha rasmi ya soko la hisa
- Mgogoro mwingine wowote unaoweza kujitokeza wakati Mamlaka inapotekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria hii.
Baraza halitakuwa na mamlaka kwenye masuala ya kijinai.
Utaratibu wa Dhamana
- Mtu yeyote ambaye hajaridhishwa na uamuzi wa Mamlaka au upande wowote kama ilivyoelekezwa chini ya Kanuni ya 7(1) ya Kanuni za Masoko ya Mitaji na Dhamana, Tangazo la Serikali Na. 649 ya mwaka 2023 anaweza kukata rufaa kwa Baraza ndani ya siki thelathini (30) kuanzia tarehe ambayo uamuzi ulifanyika.
- Utaratibu wa rufaa utaanza kwa kuwasilisha maelezo kwa maandishi kwa Msajili wa Baraza, yakielezea mgogoro husika kama ilivyoainishwa chini ya Kanuni ya 7(1).
Tangazo la Nia ya Kukata Rufaa
Mtu yeyote anayekusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mamlaka anapaswa kuwasilisha tangazo la nia ya kukata rufaa ndani ya siku saba (7) kuanzia tarehe ya uamuzi kufanyika.
Tangazo la nia ya kukata rufaa litapaswa kutimiza vigezo vifuatavyo:
- Libainishe kama rufaa hiyo inahusu uamuzi wote au sehemu mahususi za uamuzi
- Likamilishwe kwa kujaza Fomu Na. 1 ya CMT, kama ilivyoelekezwa kwenye Jedwali la Kwanza kwenye Kanuni
- Lisainiwe na mleta maombi au mwakilishi wake mwenye idhini
- Liwasilishwe kupitia nakala saba (7).
- Ada ya uwasilishaji wa tangazo la nia ya kukata rufaa itakuwa kama ilivyoainishwa kwenye Jedwali la Pili kwenye Kanuni.
- Upande wowote unaojiunga kwenye rufaa utapaswa pia kulipa ada kama ilivyoainishwa kwenye Jedwali la Pili kwenye Kanuni.
NYARAKA ZA RUFAA
Uwasilishaji wa rufaa
- Utaratibu wa kukata rufaa kwa Baraza utaanza kwa kuwasilisha Maelezo ya Rufaa kwa Msajili wa Baraza ndani ya siku thelathini (30) tangu tarehe ya uamuzi wa Mamlaka unaokatiwa rufaa.
- Maelezo ya Rufaa yataandaliwa kwa kutumia Fomu Na. 2 ya CMT, kama ilivyoelekezwa kwenye Jedwali la Tatu kwenye Kanuni.
- Kila rufaa itapaswa kujumuisha viambatanisho vyote muhimu vitakavyofanikisha kushughulikiwa kwa rufaa.
Nyaraka Muhimu
- Bila kuathiri Kanuni Ndogo ya 2, rufaa itapaswa kuambatanishwa na nyaraka zifuatazo;
- Nakala iliyoidhinishwa ya uamuzi wa Mamlaka
- Nakala iliyoidhinishwa ya mwenendo wa shauri lililoendeshwa na Mamlaka
- Nakala ya Tangazo la Nia ya Kukata Rufaa
- Maelezo ya Rufaa
- Nyaraka nyingine zozote mleta maombi atakazoona zina umuhimu katika kuhakikisha rufaa inasikilizwa kikamilifu bila upendeleo.
Katika kuzingatia Kanuni Ndogo ya 4(b), “mwenendo” si lazima ujumuishe vielelezo na viambatanishi vilivyowasilishwa wakati wa usikilizaji wa shauri kwenye ngazi ya Mamlaka.
Baraza linaweza, kwa utashi wake, kuhitaji kuwasilishwa kwa vielelezo na viambatanishi vilivyoletwa wakati wa usikilizaji wa shauri na Mamlaka.